Mabalozi watakiwa kuweka mbele maslahi ya Taifa

0
242

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuweka mbele maslahi ya Taifa wakati wote watakapokuwa wakiiwakilisha nchi katika maeneo yao.
 
 Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Rwanda, Sweden, Uturuki, Korea Kusini, Uswisi, India na Ethiopia ambao walifika kumuaga kabla ya kuelekea kwenye vituo vyao vipya vya kazi.
 
 Amewaagiza kwenda kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kukuza ushirikiano wenye manufaa baina ya Tanzania na maeneo yao ya uwakilishi hasa kwa kuweka mkazo katika diplomasia ya kiuchumi.
 
Amesema ni vema mabalozi hao kwenda kujifunza yale ambayo yanafanyika katika nchi hizo na kuhamisha maarifa hayo kwa lengo la  kukuza na kuendeleza uchumi wa Tanzania.
 
Makamu wa Rais ameongeza kuwa nchi wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania zina fursa nyingi, hivyo ni vema kutafuta fursa hizo kwa ajili ya Watanzania.
 
Pia amewataka Mabalozi hao wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kutafuta Wawekezaji watakaowekeza nchini, na hivyo kuimarisha uchumi wa Tanzania.