Mabadiliko ya sheria ya rasilimali za maji yapita

0
313

Bunge limepitisha mabadiliko ya sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji ya mwaka 2022 ambayo yanalenga kuongeza ulinzi na usimamizi wa rasilimali hizo hapa nchini.

Akisoma mabadiliko ya baadhi ya vifungu katika sheria hiyo Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameliomba bunge kufanya marekebisho katika fungu la 37 kipengele cha 4 kinachosimamia ulinzi wa rasilimali za maji.

Waziri Aweso pia ameliomba bunge kufanya mabadiliko katika sura ya 331 inayobadili cheo cha meneja wa bonde la maji na kuwa wakurugenzi wa maeneo hayo na kuwafanya kuwa maafisa masuhuli wa mamlaka hizo.

Aidha bunge pia limefanya mabadiliko katika kifungu cha 3 cha sheria hiyo ambapo sasa kitatambua Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya wilaya na Mahakama kuu kama vyombo vya kushughulikia makosa yanayotendwa chini ya sheria hizo.

Mabadiliko mengine yanahusisha fungu 44 ambalo linabainisha tofauti ya watendaji wa makosa kati ya kosa la kutumia maji bila kibali na kosa la kutumia maji kinyume na kibali.

Hata hivyo baadhi ya wabunge wametoa mapendekezo yao kuhusiana na mabadiliko ya vifungu hivyo vya sheria ili kuiwezesha serikali kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali hizo.