Maalim Seif Amgeukia Membe, Asema Mzee wa Ubwabwa anaonekana sana kuliko yeye

0
294

Mwenyekiti wa chama cha ACT-WAZALENDO, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema amesikitishwa na kitendo cha mgombea wao wa urais, Bernard Membe kuzungumza na vyombo vya habari kuwa anaendelea na kampeni.

Maalim Seif amesema uamuzi wa kumuunga mkono mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ulipitishwa na kikao cha kamati ya chama ambacho pia Bernard Membe alishiriki kwenye kikao hicho.

“Chama chetu cha ACT-WAZALENDO kupitia mkutano mkuu wa Taifa, uliamua kwamba tunataka mabadiliko katika nchi yetu na kama vyama makini havitashirikiana itakuwa ni vigumu kuiondoa CCM, kwa hiyo mkutano mkuu wa Taifa ukatoa madaraka kwamba tunashirikiana na wenzetu katika vyama ambavyo ni makini,” amesema Maalim Seif.

Aidha, amesema mpaka sasa mgombea wao hajafanya kampeni maeneo mengi ukilinganisha na mgombea wa CHAUMA, Hashim Rungwe.

“Mgombea wa Ubwabwa anaonekana kuliko mgombea wetu. Maamuzi tulifanya Membe akiwepo na akasema kama nitakuwa sijaanza kampeni nitamuunga Tundu Lissu.”

Oktoba 19, 2020 mgombea urais kupitia chama cha ACT-WAZALENDO, Bernard Membe, alijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kusema kuwa anaendelea kugombea nafasi hiyo huku akisema kuwa anaamini atashinda kinyang’anyiro hicho.