Tarehe 26 mwezi Februari mwaka huu akiwa katika ziara yake mkoani Dar es salaam, Rais John Magufuli aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza mkopo wa shilingi bilioni 12 uliotolewa na benki ya CRDB kwa halmashauri ya manispaa ya Temeke mkoani humo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Temeke kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM), -Dorothy Kilave kuomba Serikali iwasaidie kulipa mkopo huo unaowagharimu shilingi bilioni 4.8 kila mwaka.
Agizo la pili lilihusu kuchelewa kwa malipo kwa Wastaafu wa Jeshi la Polisi nchini, ambapo Rais Magufuli aliwataka viongozi wa ngazi ya juu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha malipo ya Wastaafu hao yanashughulikiwa haraka iwezekanavyo.