Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa yote nchini waimarishe mawasiliano, ili kutatua changamoto zitakazojitokeza wakati zoezi la sensa likiendelea.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakuu wa mikoa kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya mtandao, akiwa ofisini kwake Magogoni mkoani Dar es Salaam.
“Kila siku saa mbili usiku kila mkoa uwe na takwimu za siku nzima, hii itasaidia kubaini mapungufu yako wapi na kuongeza kasi kwenye maeneo ambayo yatabainika kuwa yanasuasua.” ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza kuwa
“Kamati za sensa za mikoa na wilaya nazo pia ziwe barabarani ili kufuatilia mwenendo wa sensa katika maeneo yao, hii itawapa uhakika makarani wetu wakijua kuwa mnawafuatilia.”
Pia Waziri Mkuu Majaliwa amesema ipo haja ya kudhibiti tabia ya upotoshaji inayofanywa kwenye mitandao ya jamii.
“Zungumzeni na watu wenu wa TEHAMA ili wafuatilie, pia picha zenye matumizi ya reflectors yasiyokuwa sahihi, ziachwe kusambazwa.” ameelekeza Waziri Mkuu
Amesema wakuu wa mikoa kwa kushirikiana na kamati za Sensa wahakikishe maeneo yote yanafikiwa, kaya zote zinafikiwa na watu wote wanahesabiwa.