Maagizo 5 ya Rais Samia kumaliza ajali za barabarani

0
269

Asilimia 90 ya ajali za barabarani zinazotokea nchini Tanzania husababishwa na makosa ya kibinadamu ambayo yanaweza kuzuilika.

Takwimu hizo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan akifungua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa iliyofanyika mkoani Arusha.

Rais amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza utoaji wa elimu ili kupunguza athari ambazo Taifa linapata kila mwaka kutokana na ajali hizo.

Akitolea mfano ajali za bodaboda amesema kwa mwaka  watu 400 hufariki nchini, huku 800 wakipata madhara mbalimbai kutokana na ajali hizo.

Ili kupunguza tatizo hilo, Rais Samia ametoa maagizo matano kwa Jeshi la Polisi, ambayo ni;

Kuongeza utoaji elimu ya usalama barabarani kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kila mtumiaji wa barabara azifahamu taratibu.

Licha ya  kuongezeka kwa vipindi vya redio na televisheni, Rais amelitaka jeshi hilo kutumia zaidi mitandao ya kijamii kwani vijana ambao ni walengwa wakubwa wakati mwingine hawatazami televisheni wala kusikiliza redio.

Pili, ameagiza utafiti kufanyika ili kuwezesha kupatikana kwa suluhu ya kisayansi ya kupunguza ajali barabarani. Ameelekeza hilo kufanyika kwa kushirikiana na vyuo mbalimbali nchini.

Tatu, amewataka askari polisi wawe chanzo cha usalama barabarani kwa kuhakikisha kunapokuwa na tatizo, wananchi wanawakimbilia na sio kuwakimbia.

Amesema wakati mwingine madereva huwakimbia askari polisi, na mwishoe huishia kupata ajali.

Nne, ameelekeza polisi kutokushikilia leseni za madereva kinyume na sheria, huku akiagiza polisi kutokuwalazimisha madereva kulipa faini papo hapo wanapokamatwa. Ameeleza kushangazwa na vyombo vingi vya usafiri, mathali pikipiki ambazo zimejazana kwenye vituo vya polisi, na hivyo kutaka lifanyiwe kazi, kesi au faini ikilipwa ziachiwe.

Mwisho, amewataka wananchi kuchukua wajibu wa kuzuia ajali kwa kuzingatia sheria za barabarani wanapotumia vyombo vya moto na kutoa taarifa pindi mtumiaji mwingine anapovunja sheria.

Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani imeanza leo Novemba 23 hadi 28, 2021, ambayo huambatana na utoaji wa elimu kuhusu usalama wa barabarani pamoja na ukaguzi wa magari.