Maafisa habari wizarani watakiwa kuimarisha uhusiano na wanahabari

0
308

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewataka maafisa habari za wizara zote kuimarisha mahusiano na waandishi wa habari ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Msigwa ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma alipokutana na wakuu wa vitengo vya mawasiliano serikalini kutoka wizara zote kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kuboresha vitengo hivyo katika utoaji wa taarifa za serikali.

“Tafuteni namna nzuri za kushirikiana na vyombo vya habari, mkiimarisha mahusiano mazuri na waandishi wa habari, mtafanya kazi zenu kwa urahisi,” ameagiza Msigwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi (Mawasiliano Serikalini) wa Idara hiyo, Zamaradi Kawawa amewataka maafisa hao kuimarisha mahusiano na wadau wao wote.

“Tuwe na mahusiano mazuri miongoni mwetu, pia baina yetu na watumishi wenzetu wa wizara zetu na wizara nyingine.”

Mwaka 2005 Serikali ilianzisha vitengo vya mawasiliano serikalini na mwaka 2016 serikali ikapitisha Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ili wanahabari na wananchi wapate taarifa za utendaji kazi wa Serikali kwa urahisi.