Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya maafisa elimu wa mikoa na wilaya nchini wanaoshirikiana na walimu kujihusisha na wizi, udanganyifu na uvujaji wa mitihani, waache mara moja tabia hiyo, vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa onyo hilo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Sita wa Umoja wa Maafisa Elimu wa mikoa na wilaya(REDEOA), mkutano wenye kaulimbiu inayosema kuwa Elimu Bora Itatufikisha Katika Uchumi wa Kati Ifikapo mwaka 2025.
“Kamati za mitihani za mikoa na wilaya ziendelee kusimamia sheria, kanuni na taratibu bila ya woga, upendeleo na tusiyumbishwe na hatua za kinidhamu na kiutumishi kwa mujibu wa sheria, hatua ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wote wanaobainika kukiuka sheria, taratibu na miongozo inayotolewa”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amewapongeza maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya nchini kwa kufanya kazi kubwa ambayo imechangia kupandisha ufaulu wa kidato cha Nne na cha Sita na amewataka waendelee kufanya kazi kwa bidii.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ambaye amewataka maafisa hao wawe wanatoa taarifa sahihi kuhusu idadi ya wanafunzi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.