Lukuvi: Shusheni majukumu ya usimamizi wa ardhi kwenye mitaa/vijiji

0
331

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha wanashusha usimamizi wa masuala ya ardhi katika ngazi za mitaa na vijiji ili ziweze kuepuka ujenzi holela na kurahisisha ufuatiliaji wa makusanyo ya kodi ya pango la ardhi.

Akizungumza wakati akikagua ofisi ya ardhi katika halmashauri ya manispaa ya Singida, Waziri Lukuvi amesema ni vema Wakurugenzi wa halmashauri nchini wakawapa kazi watendaji wa mitaa na vijiji ya kusimamia masuala ya ardhi.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi amesema watendaji wa mitaa na vijiji watakaokasimia masuala ardhi katika maeneo yao hawatakuwa na jukumu la kugawa, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, bali kuangalia yanayoendelea katika mitaa yao na wakikuta ukiukwaji wowote kama vile ujenzi holela basi watakuwa na wajibu wa kusitisha.

”Afisa ardhi katika wilaya hawezi kujua yale yanayoendelea kwenye mtaa au kijiji na hata suala la kodi, mkiwatumia watendaji wa mitaa wataweza kusaidia kuwabaini wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi kirahisi,” amesema Waziri Lukuvi.

Ametaka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri nchini kuhakikisha wanatengeneza majedwali maalum yenye orodha inayoonesha kila mmiliki wa kiwanja, kwa lengo la kuwawezesha watendaji wa mitaa kuwajua wamiliki katika maeneo yao.