Lishe bora mwarobaini wa matatizo ya afya

0
195

Mikoa 15 nchini Tanzania ikiwemo inayozalisha kiwango kikubwa cha chakula kama vile Kagera, Njombe, Mbeya na Iringa imebainika kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu na utapiamlo, tatizo linalotokana na ukosefu wa baadhi ya virutubisho kutokana na kula zaidi aina moja ya vyakula.

Hayo yameelezwa na mtaalamu wa lishe, Dkt. Daniel Nyagawa kwenye semina ya kuwajengea uwezo Kikundi cha Wabunge Vinara wa Usalama wa Chakula iliyofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, ambapo kufafanua kuwa, matatizo hayo yanazigharimu familia na Taifa kutokana na kukosa nguvu kazi imara na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu.

Licha ya kuwepo vyakula katika mikoa hiyo, lakini amesema chanzo cha udumavu kinatokana na wananchi kula aina fulani tu za vyakula, hivyo mwili kukosa virutubisho muhimu za kufanya makuzi ya mtoto kuwa na mapungufu.

Ameongeza kuwa, watu kutokupata lishe bora, kumekuwa kukichangia pia upungufu wa nguvu za kiume, na kwamba kama tatizo ni ukosefu wa virutubisho fulani, hata ukitumia miti shamba, au dawa nyingine yoyote hauwezi kupata suluhisho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi hicho, Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira amesema imekuwa semina nzuri ambayo imewajengea uwezo kuhusu masuala ya lishe, hususani lishe kwa vijana balehe wa kike, hali ya lishe nchini na nafasi ya wabunge katika kutatua changamoto hiyo.

Mambo ambayo tumekubaliana kwamba mwaka 2022 tiyabebe ni, “namna gani ajenda ya lishe inapewa kipaumbele na wizara za kisekta, ikiwemo pia kutengewa bajeti. Pia, namna gani sehemu ya fedha inayotokana na mauzo ya vyakula vyenye chumvi, mfuta, sukari inatumika kuimarisha masuala ya lishe kwa Taifa,” ameeleaa Neema.