Lazima tutambue kilimo ni Sayansi

0
149

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametoa tahadhari ya kuwepo kwa mtindo wa kubadili matumizi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na kuelekeza kupimwa kwa maeneo hayo.

Akifungua rasmi sherehe na maonesho ya kimataifa ya wakulima Nanenane mwaka 2023 mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale amesema kumekuwepo na mtindo wa kubadili matumizi ya ardhi yaliyotengwa mahsusi kwa ajili ya tafiti za kilimo ambapo maeneo hayo yamevamiwa na baadhi kupimwa viwanja vya makazi.

Dkt. Mpango amesema mtindo huo unatishia utafiti wa kilimo na mifugo kwa kuwa vituo vya utafiti vilivyopo katika maeneo hayo vitakosa nafasi yakutosha ya kufanyia shughuli za tafiti.

Amesema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa kilimo ni sayansi, kilimo kinapaswa kuhusisha utafiti hivyo ikiwa hapatakuwa na kipaumbele katika kutunza maeneo ya tafiti hizo ni uhakika kuwa mapinduzi ya kilimo yanayotamaniwa kwa muda mrefu yatasalia kuwa ndoto.

Aidha, Dkt. Mpango ameelekeza mamlaka husika kuhakikisha maeneo hayo yanapimwa, yanapewa hatimiliki na yanapewa ulinzi. Amesema taasisi zinazosimamia maeneo hayo zisiache maeneo hayo bila kutumika.