Mkuu wa Kimila wa kabila la Wamasai waliokuwa wakiishi katika Hifadhi ya Ngorogoro, Laigwanani Matigoi Tauwo amemshukuru Mungu kwa kumuongoza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuwapatia makazi bora katika kijiji cha Msomera kilichopo wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Akishukuru kwa niaba ya wananchi wenzake wa Ngorongoro ambao wameamua kuhama kwa hiari, Laigwanani Tauwo amesema sasa maisha yao yatakuwa ya amani zaidi na yenye maendeleo kuliko huko nyuma kwa kuwa serikali imewapatia nyumba, ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji, pia huduma bora za kijamii kama elimu na afya.
“Namshukuru sana Mungu kwa kutupa Rais Mama Samia, leo sisi tunamiliki nyumba jamani, kweli Mungu mkubwa sana, tunaahidi tutaishi vizuri sana na ndugu zetu wa hapa Msomera.” amesema Laigwanani Tauwo.
Katika zoezi la kuwapokea wananchi hao walioamua kuhamia kijiji cha Msomera ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Ngorongoro, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana amewakabidhi wananchi hao hati za ardhi zilizotolewa na wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.