Kunenge: Dar yatoa heshima ya juu kwa JPM

0
168

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, -Aboubakar Kunenge amewashukuru Wakazi wa mkoa huo kwa kujitokeza kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli.

Kunenge amesema kuwa, wingi wa watu waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho unathibitisha kuwa Marehemu Rais Magufuli alikuwa ni kipenzi cha watu wa Dar es salaam na kwamba hiyo ni heshima ya juu kwa kiongozi huyo.

Akizungumza na Waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kukamilika kwa shughuli ya kuusafirisha mwili wa Dkt Magufuli kwenda mkoani Dodoma, Kunenge amesema Wakazi wa Dar es salaam wamemtendea haki Marehemu Dkt Magufuli kwa namna walivyojitokeza.

Kunenge ameongeza kuwa Wakazi wa Dar es salaam wameguswa na maisha ya Dkt Magufuli, ndio maana wamejitokeza kwa wingi kumpa heshima yake katika siku zote mbili walizopewa nafasi ya kumuaga katika uwanja wa Uhuru.

Mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli tayari umewasili mkoani Dodoma kwa ajili ya shughuli ya kitaifa la kuuaga itakayofanyika hapo kesho.