Kodi ya ardhi kwa taasisi za dini yafutwa

0
1028

Serikali imefuta kodi ya pango ya ardhi kwa taasisi na madhehebu ya dini nchini kuanzia mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Hatua hiyo imetangazwa jijini Mbeya na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, – William Lukuvi wakati wa ibada ya kuwaweka Wakfu viongozi wa Jumuiya Kuu ya Kanisa la Kibaptisti Tanzania (BCT).

Akitangaza hatua hiyo,  Waziri Lukuvi amesema  kuwa Rais  John Magufuli ameiagiza wizara hiyo kutoyatoza kodi madhehebu ya dini kwa sehemu ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya kufanyia ibada.

“Rais ameagiza kuanzia Julai mosi mwaka huu wa fedha,  madhehebu ya dini yasilipe kodi ya ardhi kwa maeneo ambayo huduma za maombi na ibada zinatolewa, hata hivyo msamaha huu hauhusu maeneo ambayo kuna miradi ya kuingiza fedha ambayo tunajua madhehebu mengi yameanzisha,” amesema Waziri Lukuvi.

Amefafanua kuwa tayari agizo hilo limetolewa kwa Makamishna wa ardhi wa kanda na mikoa pamoja na maofisa ardhi wa majiji, manispaa na halmashauri  zote nchini.

Hata hivyo,  Waziri Lukuvi ametoa nafasi ya kukutana na viongozi wa dini ambao wana migogoro ya ardhi kwenye maeneo ambayo wanatoa huduma.

“Najua kuna migogoro mingi kwenye maeneo ambayo mnatoa huduma,  hivyo nawakaribisha ofisini kwangu Dodoma na kama migogoro itakuwa mikubwa nitafika mpaka eneo la mgogoro,” amesema Waziri Lukuvi.

Awali, Askofu wa kanisa la Baptisti nchini, Arnold Manase alimweleza Waziri Lukuvi kuwa kanisa  hilo ni moja ya madhehebu yanayoongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi.


“Kwa kuwa Waziri mwenye dhamana upo, naomba nafasi nije ofisini kwako nikueleze migogoro iliyopo ndani ya kanisa langu ili uangalie namna ya kuitatua maana migogoro imekithiri mpaka kufikia hatua ya kujenga makundi miongoni mwa waumini,” amesema Askofu Manase.