Rais Samia Suluhu Hassan leo amezindua mtambo wa kusafisha dhahabu mkoani Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery Limited) akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara mkoani humo.
Kiwanda hicho ambacho umegharimu shilingi bilioni 12.2 kitaongeza mapato ya Serikali kupitia mrabaha, tozo za ukaguzi na ushuru wa huduma na kutoa ajira za moja kwa moja 120 na zisizo za moja kwa moja 400.
Aidha, mtambo huo utachochea ukuaji wa uchumi kwa kuiwezesha Benki Kuu ya Tanzania kununua dhahabu na hivyo kuwezesha nchi kuwa na amana ya dhahabu kwa kiwango kikubwa.
Mbali na hilo, mtambo huo utasaidia kuchochea shughuli za uchimbaji madini kwenye Ukanda wa Ziwa.
Akizungumza na wananchi, Rais Samia Suluhu Hassan amesema mtambo huo na mingine miwili iliyopo nchini ni matokeo ya mabadiliko ya sheria iliyofanywa na Serikali katika sekta ya madini ambayo imeongeza mapato ya madini kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 528 mwaka 2020.
Mafanikio mengine yanayopatikana kufuatia mabadiliko ya sheria ya madini nchini ni kuanzishwa kwa masoko 39 na vituo 50 vya kuuzia madini, kutolewa kwa leseni nne za usafishaji madini ya dhahabu katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Geita.
Wakati huo huo, Rais ameitaka Wizara ya Madini kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini ikiwemo kudhibiti wizi, utoroshaji na biashara ya magendo pamoja na kusimamia mgodi wa Tanzanite uliopo Mererani ili Tanzanite inayozalishwa nchini pekee iweze kuwa na manufaa zaidi kwa taifa.