Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam wanaotumia kivuko kwenda na kutoka Kigamboni mkoani Dar es Salaam wamesema kwa muda wa siku ya tatu sasa wanapata adha ya kukaa kituoni kivukoni (feri) kwa zaidi ya saa moja kufuatia kupata hitilafu kwa kivuko cha MV. Magogoni.
Wakazi hao wameelezea adha hiyo wakati wakizungumza na mwandishi wa TBC na kuongeza kuwa, changamoto hiyo ya usafiri pia inahatarisha usalama wao.
Taarifa ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa vyombo vya habari imekiri kivuko hicho cha MV. Magogoni kushindwa kutoa huduma kutokana na kupata hitilafu kwenye mifumo ya uendeshaji, na hivyo kusababisha huduma kusimama.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mafundi wa TEMESA wanaendelea kurekebisha mifumo ya mitambo ya uendeshaji iliyoathirika, ili kurudisha huduma za kivuko haraka iwezekanavyo.
Kwa sasa shughuli za uvushaji abiria kwenda na kutoka Kigamboni zinaendelea kwa kutumia kivuko cha MV. Kigamboni.