Kituo cha huduma kwa pamoja huko Namanga chazinduliwa

0
1664

Rais  John Magufuli na Rais  Uhuru Kenyatta wa Kenya wamezindua kituo cha huduma kwa pamoja mpakani katika eneo la Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Pamoja na kuzindua ofisi za kituo hicho katika pande zote mbili,  Marais hao wamepanda miti ya kumbukumbu na kukagua utoaji wa huduma zikiwemo za forodha na uhamiaji.

Kituo hicho ni miongoni mwa vituo 15  vinavyojengwa katika mipaka ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa lengo la kurahisisha ufanyaji wa biashara miongoni mwa nchi hizo, kuharakisha huduma za mpakani, kuongeza mapato na kuimarisha usalama.

Ujenzi wa kituo hicho cha huduma kwa pamoja mpakani katika eneo la Namanga umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Serikali za Tanzania na Kenya ambapo miundombinu ya upande wa Tanzania imegharimu shilingi Bilioni 22.365.

Tangu kianze kutoa huduma,  kituo hicho kimesaidia kupunguza muda unaotumiwa kukamilisha huduma za mpakani  kutoka saa moja hadi dakika 15, na pia kwa upande wa Tanzania ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka shilingi Bilioni 41 hadi kufikia shilingi Bilioni 58 zinazotarajiwa mwaka huu.

Wakizungumza baada ya kuzindua kituo hicho Rais Magufuli na Rais Kenyatta wamewashukuru wafadhili wa ujenzi huo na wametoa wito kwa Watanzania na Wakenya kuongeza biashara kupitia mpaka huo, huku wakitaka wafanyabiashara wadogo wasibughudhiwe.

“Kenya ni ya tatu kati ya nchi 10 zinazoongoza kwa uwekezaji Tanzania, kwa hiyo Wafanyabiashara wa Kenya wanapopita hapa msiwaone kuwa ni maadui, halikadhalika Tanzania ni yenye mifugo mingi hasa ng’ombe kwa hiyo Watanzania wanapopeleka nyama Kenya nao wasikwamishwe” amesisitiza Rais Magufuli.

“Sisi tujione wana Afrika Mashariki, tuzilete nchi zetu pamoja na tuutumie umoja wetu wa watu takribani Milioni 200 kufanya biashara na kunufaika, sisi viongozi wajibu wetu ni kurahisisha biashara sio kukwamisha, na nyie wananchi muwe huru kufanya biashara zenu ilimradi msivunje sheria na kufanya biashara haramu” amesema Rais Kenyatta.

Aidha, Rais Magufuli ameahidi kushughulikia tatizo la maji katika eneo la Namanga kwa kupeleka maji  kutoka Longido ambako serikali imejenga mradi mkubwa wa maji uliogharimu shilingi Bilioni 15.

Rais Magufuli pia ameishukuru AfDB baada ya Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki, – Gabriel Negatu kueleza kuwa benki hiyo imeridhia kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Malindi – Lungalunga – Tanga – Pangani – Bagamoyo inayounganisha nchi za  Tanzania na Kenya, na mradi wa barabara ya Rumonge – Manyovu – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi inayounganisha nchi za Tanzania na Burundi.