Kitabu cha The Game Changer : President Magufuli’s First Term In Office hadharani

0
142

Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelee kutoa elimu ya uchumi wa viwanda kwa Wananchi, ili waweze kushiriki kikamilifu kujenga na kukuza uchumi huo.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kitabu cha The Game Changer : President Magufuli’s First Term In Office, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kwamba Wawekezaji wanaweza kuwekeza nchini bila vikwazo vyovyote.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kitabu hicho kimefafanua kuwa Tanzania ni nchi yenye kuendeshwa Kidemokrasia na kimeondoa shaka waliyonayo Wadau wa maendeleo na Wawekezaji.

Kitabu hicho pia kinaeleza mabadadiliko aliyoyafanya Rais Magufuli kwa nchi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Wakizungumza katika uzinduzi wa kitabu hicho, Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Utafiti ya Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki na Kusini ( ESAURP) Ruta Mutakyahwa pamoja na Mhariri Mkuu wa kitabu hicho  Profesa Ted Maliyamkono wamesema kuwa kitabu hicho kinaonesha muelekeo wa nchi tangu Rais Dkt John Magufuli alipoingia madarakani.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ambaye ndiye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma amesema uzinduzi wa kitabu hicho ni kumbukumbu nzuri kwa vizazi vijavyo kufahamu mabadiliko yaliyofanyika hapa nchini.

Kitabu hicho cha The Game Changer : President Magufuli’s First Term in Office chenye kurasa 641 na sura 30 kimeandikwa na waandishi zaidi ya arobaini na kuhaririwa na Profesa Ted Maliyamkono na Dkt Hugh Mason.