Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amewashauri viongozi na wataalamu wa serikali kuacha kutoa ahadi ambazo wanajua hazitatekelezeka au utekelezaji wake utachukua muda mrefu.
Amesema ahadi hizo ‘hewa’ zimekuwa zikikwamisha shughuli za maendeleo na kusababisha malalamiko kwa wananchi.
Kinana ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Bunda Mjini mkoani Mara baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuwa serikali iliwataka wahame katika maeneo yao kupisha ujenzi wa mradi wa maendeleo uliochukuwa muda mrefu.
Wananchi pia walielezea pia kukerwa na kitendo cha maeneo yao kuchukuliwa, nyumba kubomolewa na kupewa sharti la kutoendeleza maeneo, hususani katika Kijiji cha Nyantwale.
“Viongozi wa serikali, kabla ya kuwahamisha wananchi ni vema wakaeleza ni lini ahadi hiyo itatekelezwa, kama ni fidia, lini fidia hiyo itatolewa, kama ni watu kuhama watahama lini, kama watu ni kupewa fidia watapewa lini (badala ya kuwazuia kuendeleza maeneo ya kwa kipindi kisichojulikana),” amesema.
Amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kutoa ahadi ambayo inachukua miaka mingi kutekelezwa huku kila kiongozi anayekuja akitoa ahadi na kuishia zake.