Kinana : Kiswahili kilitumika kama lugha ya mapambano

0
184

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amesema lugha ya kiswahili imekuwa na mchango mkubwa katika ukombozi wa Bara la Afrika, kwani lugha hiyo ilitumiwa na viongozi wengi katika kuwasiliana na kutoa amri za mapigano.

Kinana ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani yaliyobeba kaulimbiu inayosema Kiswahili ni Chachu ya Maendeleo na Utangamano Duniani.

“Walimu wengi wakuu katika majeshi ya Afrika walikuwa ni Watanzania, hivyo majeshi ya nchi nyingi yalilazimika kujifunza kiswahili, mfano FRELIMO na ZANU – PF walitumia lugha ya Kiswahili katika kutoa amri kama vile kaa chini, simama juu.” amesema Kinana

Amesema lugha ya Kiswahili ilitumika kama lugha ya wamasiliano katika ukombozi wa Afrika ili kuwafanya wakoloni wasielewe malengo ya Afrika.

Aidha Kinana ameongeza kuwa pamoja na mchango wake katika ukombozi wa Bara la Afrika, Kiswahili pia kimesaidia kuimarisha ushirikiano na ujirani mwema kwa nchi za Afrika Mashariki kama vile Kenya na Uganda.

Katika kuadhimisha siku ya Kiswahii Duniani, Kinana ametoa wito kwa wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo chini ya Waziri Mohamed Mchengerwa kutumia fursa zilizopo duniani kufungua soko la ajira, kwenda kufundisha Kiswahili duniani pamoja na Watanzania kuchangamkia fursa za kufanya kazi kwenye vyombo vya habari duniani vinavyotangaza kwa lugha ya Kiswahili.