Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amewahimiza wanachama wa CCM kuwa wamoja na kujenga mshikamano ili kwenda katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2025 wakiwa wamoja na kuibuka washindi.
“Nipongeze kazi kubwa inayofanywa na viongozi wa CCM hususani katika ngazi ya kitongoji, kijiji, mtaa na kata. Mwakani ni mwaka wa uchaguzi, hivyo naamini wana CCM tutakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mtaa mwaka 2024 tukiwa kitu kimoja,” amesema Kinana.
Akizungumza leo Julai 23, 2023 kwenye kikao cha ndani cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa chama pia kinatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotelewa na viongozi wa CCM katika ngazi za kata, vitongoji, vijiji, wilaya na mkoa kwani wao ndio wanaokutana na wananchi na wakati wa uchaguzi ndio wanaokwenda kuomba kura.
Pia, amewapongeza madiwani wanaotokana na CCM ambao wamekuwa wakisimamia ngazi ya kata na wamekuwa wakifanya hivyo bila ya kuwa na mshahara lakini wameendelea kujitoa kuwatumikia wananchi.