Kimbe akabidhi mali za ofisi ya Meya Iringa

0
343

Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe amekabidhi ofisi na kurejesha gari la serikali alilokuwa akilitumia huku akiahidi kuendelea kushirikiana na manispaa katika shughuli za maendeleo.

Akiwaaga watumishi katika ukumbi wa manispaa hiyo, Kimbe aliyeondolewa madarakani na madiwani Jumamosi iliyopita amesema hana kinyongo na anakubaliana na maamuzi.

Kiongozi huyo ameachia ngazi baada ya madiwani kupiga kura ya kutokuwa na imani naye kwa kumtuhumu kwa matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

Kimbe amesema ameomba kukutana na watumishi hao awaage na awashukuru kwa ushirikiano walioutoa katika kipindi cha miaka minne aliyotumikia manispaa kama meya.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Hamid Njovu amekiri kukabidhiwa ofisi na gari la ofisi ya meya na kumshukuru kwa ushirikiano alioutoa.