Kiini cha matukio ya moto GESECO hadharani

0
211

Jeshi la Polisi mkoani Geita limebaini chanzo cha matukio ya moto katika shule ya sekondari ya Geita (GESECO) ni ugomvi wa muda mrefu baina ya Wanafunzi wa kutwa na bweni, ambapo Wanafunzi wa kutwa wanadai uongozi wa shule hiyo umekuwa ukiwapendelea Wanafunzi wa bweni hasa katika masuala ya chakula.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe ameyasema hayo mbele ya Waandishi wa habari mkoani Geita,  alipokuwa akitoa taarifa ya uchunguzi wa matukio ya moto yaliyotokea shuleni hapo tarehe 5, 6 na14 ya mwezi huu.

Ameongeza kuwa mbali na matukio ya moto shuleni hapo, shule hiyo pia imekuwa na historia ya kuwa na Wanafunzi watukutu, wavuta bangi na waharibifu.

Kufuatia matukio hayo ya moto katika shule ya sekondari ya Geita, Kamanda huyo wa polisi mkoani Geita amewataka Wanafunzi wote mkoani humo kutojihusisha na vitendo vya uhalifu wawapo shuleni na badala yake wazingatie masomo, na amewataka Wazazi kufuatilia mienendo na tabia za watoto wao wawapo shuleni.