Kigoma kuunganishwa na Gridi ya Taifa

0
262

Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anaendelea na ziara yake ya siku nne mkoani Kigoma amesema umeme wa majenereta mwisho kesho mkoani humo, kwani atakwenda kuzima majenereta hayo akiwa wilayani Kasulu.

Amesema mara baada ya kuzima majenereta hayo hapo kesho, Kigoma itaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, huku ikipokea umeme kutoka vyanzo sita vya umeme alivyovizindua hii leo wakati akiwa kwenye ziara yake mkoani humo.

Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi wa Kigoma kwa nyakati tofauti alipokuwa akizindua barabara ya Nyakanazi – Kabingo yenye urefu wa kilomita 50 iliyojengwa kwa kiwango cha lami, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kibondo Town link yenye urefu wa kilomita 25.9, kuzindua mradi wa maji na uzinduzi wa hospitali ya wilaya ya Kakonko ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 2.9.

Aidha, Rais Samia amesema serikali inaamini kuwa miundombinu inayoendelea kujengwa mkoani Kigoma itakuwa ni ufunguo wa uchumi kwa wananchi wa mkoa huo, kwa kuwa wataunganishwa na mikoa jirani pamoja na nchi jirani kama Rwanda na Burundi.

Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea na ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Kigoma, ambapo hapo kesho atatembelea wilaya ya Kasulu.