Kifafa na Imani za kishirikina

0
351

Mara kadhaa wagonjwa wa kifafa wamekuwa wakikosa hudumu stahiki kutoka kwa jamii inayowazungukwa kutokana na dhana potofu juu ya ugonjwa huo na kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa wa kifafa.

Kifafa ni maradhi yanayoathiri sehemu ya ubongo na kuusababisha kushindwa kufanya kazi kwa mpangilio unaotakiwa.

Zipo nyakati ambapo mgonjwa wa kifafa anapoanguka kwa degedege wanaomzunguka huanza kusali, kufanya dua na wengine kwenda kuaguliwa. Imekuwa ni nadra kuona mtu akitegemea maombi au kuaguliwa pale anapopata homa za magonjwa mengine kama malaria bali hupelekwa hospitali ila kwa ugonjwa wa kifafa imekuwa ni tofauti.

Haya yamebainishwa na Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa fahamu na ubongo kwa watoto, Dkt. Edward Kija ambaye ameeleza kuwa wazazi au walezi wana mchango mkubwa sana wa kuwasaidia wagonjwa wa kifafa hususani watoto kwa kuwapeleka hospitali pale wanapoonesha dalili za kifafa kwa mara ya kwanza na kuacha kutegemea imani peke yake.

Dalili za ugonjwa wa kifafa ni pamoja na kupatwa na degedege (hali ya kudondoka, kukakamaa mwili na kutoa mapovu mdomoni) japo si wote wenye degedege huwa na ugonjwa wa kifafa kwani inaweza kuwa ni sababu ya homa kali kama malaria, homa ya uti wa mgongo, kiharusi au uvimbe katika ubongo.

Kwakuwa ugonjwa wa kifafa hutisha sababu ya dalili zinazoonekana kama mgonjwa kukakamaa, kutoa macho, kupoteza fahamu, kuanguka chini, kutoa mapovu mdomoni na kukoroma jamii imekuwa ikihusisha ugojwa huu na imani za kishirikina kuwa mgojwa kalogwa hivyo hali hii huletwa umuhimu wa kutoa elimu ya ugonjwa huu kwa jamii.

“Tunapatiwa mgonjwa ushauri na elimu juu ya ugonjwa wa kifafa ili afahamu ni kwanini anaanguka na kukakamaa… ndio sababu wengi wanaamini ni ushirikina umefanyika. Tunawaonesha picha na kumuelewesha tatizo lake limetokea sehemu ipi ya ubongo ndio sababu anapata dalili hizi ambazo eneo hilo la ubongo kazi yake ni kufanya kiungo fulani cha mwili wake kifanye kazi,” ameeleza Dkt. Kija

Kija ameongeza kuwa wagonjwa wanaowasili kupata huduma hospitalini wanakuwa wamecheleweshwa kupata huduma hizo kwa sababu zinazohusishwa na imani za kishirikina. Wengine huenda wakiwa wamevalia vitu vinavyodaiwa kuwa vya kiimani kwenye miili kama vile vitambaa vyeusi kiunoni, miguuni au mikononi ambavyo hufungiwa majani ya mvuje, mavi ya tembo au fisi ama mbegu za bangi na wakati mwingine mkojo wa binadamu.

Anasema kwanza hufanya mahojiano na ndugu za wagonjwa au mgonjwa mwenyewe na huwa wanakiri kujihusisha na imani hizo.

Dkt. Kija anasisitiza kuwa ni jambo la muhimu kuwatambua wagonjwa hawa iwapo wanajihusisha na imani hizi kusudi iwe rahisi kupokea matibabu ya hospitalini mara baada ya kuwapa elimu kuhusu kifafa.
wale ambao wamepata degedege kwa mara ya kwanza wanapatiwa elimu kusudi wasihangaike kwenda kwa waganga kwani wakichelewesha matibabu hali zao huzidi kuwa mbaya zaidi na baadaye kushindwa kutibika.

Madhara mengine yanayoweza kujitokeza ni pamoja na watoto kushindwa kuendelea na masomo, watu wazima kushindwa kuendelea na kazi na wengine hata kukosa wenzi kwasababu za unyanyapaaji.

Ikiwa mgonjwa atapatiwa matibabu mapema na kutumia dawa inavyoelekezwa na wataalamu wa afya anaweza kupona na kutopatwa na degedege.