Jumla ya watahiniwa 566,840 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne na maarifa unaotarajiwa kuanza hapo kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Athumani Amasi amesema, mtihani huo utafanyika katika jumla ya shule 5,212 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 1,794.
Amesema kati ya watahiniwa 566,840 waliosajiwa kufanya mtihani huo watahiniwa wa shule ni 535,001 na watahiniwa wa kujitegemea ni 31,839.
Kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 247,131sawa na asilimia 46.19 na wasichana ni 287,870 sawa na asilimia 53.81 huku wenye mahitaji maalumu wakiwa 852.
Kwa mujibu wa NECTA,
maandalizi yote kwa ajili ya kufanyika mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani na vijitabu vya kujibia mitihani.
Pia limezitaka kamati za mitihani katika mikoa yote kuhakikisha taratibu zote za uendeshaji mitihani ya kitaifa zinazingatiwa ipasavyo.