Kesi ya Mdee na wenzake 18 kusikilizwa leo

0
142

Wabunge wa viti maalum Halima Mdee na wenzake 18, leo wamefika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusikiliza shauri lao la kupinga uamuzi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwavua uanachama wa chama hicho.

Julai 29 mwaka huu, mahakama iliwataka Mdee na wenzake saba kufika mahakamani Agosti 26 wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano na mawakili wa CHADEMA.

Jaji Cypirian Mkeha ambaye anasikiliza shauri hilo alitoa amri hiyo dhidi ya kina Mdee kufuatia ombi lililotolewa la mawakili wa CHADEMA wakiongozwa na Peter Kibatala kuomba Mdee na wenzake saba waitwe ili waweze kuwafanyia mahojiano.

Katika shauri hilo namba 36 la mwaka 2022, Mdee na wenzake wanaowakilishwa na mawakili Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashu, wanaiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi wa CHADEMA kuwafukuza kisha itoe amri tatu.

Amri hizo ni ya kutengua mchakato wa uamuzi wa CHADEMA kuwavua uanachama wateja wao, kuilazimisha CHADEMA kutimiza wajibu wake kisheria yani kuwapa haki ya kusikiliza na amri ya zuio dhidi ya Spika wa Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapotolewa uamuzi.