Taarifa na Happyness Hans
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), Dkt. Suleiman Jafo, amesema kero chache takribani nne ambazo zimebaki kwenye muungano unaofikisha miaka 60, zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati akielezea mafanikio ya wizara yake katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na kuelekea kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya muungano.
Ametaja kero zilizobaki kuwa ni pamoja na ya mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Nyingine ni mgawanyo wa faida kutoka Benki Kuu pamoja na suala zima la uingizwaji wa sukari inayozalishwa katika kiwanda cha Mahonda cha Zanzibar katika soko la Tanzania Bara.
Amesema kero zote hizo kwa sasa zipo katika utekelezaji na kwamba katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia ufanisi umekuwa mkubwa kwa sababu zaidi ya nusu ya kero za muungano zimetatuliwa katika kipindi hiki.
“Ufanisi umekuwa mkubwa sana. Nilitoa takwimu hapo mwanzo kwamba kipindi hiki tumeweza kutatua takribani kero 15 za muungano. Hili si jambo dogo kwa kipindi cha miaka mitatu kuweza kufanikisha haya,” amesema Jafo.