Kati ya vifo vinne, kimoja ni tatizo la afya ya akili

0
267

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema wizara na Serikali imeweka mkazo katika afya ya akili ikiamini kwamba hakuna afya bila kuwa na afya ya  akili.

Akifungua Mdahalo wa Kitaifa wa Afya ya Akili mkoani Dar es Salaam, Waziri Ummy amesema ili mtu atafsiriwe kuwa ana afya kamili, lazima awe vizuri katika ustawi wa kimwili, kiakili na kijamii.

Aidha, mkazo huo unatokana na uhalisia kuwa afya ya akili ina mchango mkubwa katika uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa, hivyo athari katika akili inaathiri uwezo wa watu kujishughulisha katika shughuli za kiuchumi.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), kati ya watu nane, mtu mmoja ana tatizo la afya ya akili.

Waziri Ummy amesema kuwa nchini Tanzania watu milioni 7 wana tatizo la afya ya akili ikiwemo kutumia dawa za kulevya huku tatizo kubwa zaidi likiwa ni sonona, linalowasumbua Watanzania milioni 1.5.

Ameongeza kuwa, tatizo hilo limekuwa likigharimu maisha ya watu, ambapo kati ya vifo vinne, kimoja kinatokana na tatizo la afya ya akili.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, ametoa wito tatizo hilo lionekane kama magonjwa mengine, wagonjwa wasinyanyapaliwe kwa kuitwa vichaa, ili kuwa na mwamko wa kupata matibabu.