Katavi yawa lango la biashara

0
167

Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga – Mpanda kumefungua fursa za uchumi, ambapo wananchi kwa sasa wanasafirisha bidhaa kiurahisi kutoka mkoani humo kwenda mikoa mingine na nchi jirani.

Mrindoko amesema tangu kuanzishwa kwa mkoa wa Katavi, serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji, lengo likiwa ni kurahisisha shughuli za kiuchumi.

Amesema kwa sasa mapato mkoani Katavj yameongezeka kufuatia maboresho makubwa yaliyofanywa katika miundombinu ya usafirishaji.

Mkuu huyo wa mkoa wa Katavi ameyasema hayo alipokuwa akisoma taarifa ya mkoa wakati wa uzinduzi wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa kilomita 342.9, uzinduzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mrindoko ameongeza kuwa Wakazi wengi wa Katavi wanajishughulisha na kilimo, ambapo mazao yao kwa sasa yanasafirishwa nje ya mkoa kiurahisi na wanapata faida kubwa tofauti na ilivyokuwa awali.

“Kutokana na kukamilika kwa barabara hii tumeanza kupata faida ya usafirishaji mkoani kwetu kwa mara ya kwanza kwenye bandari yetu ya Kalema tumepokea meli kubwa ya mzigo wa madini ya Gelena kutoka Congo ambapo watatumia barabara hii kusafirisha na hii tunaamini bandari yetu itatumika kusafirisha mizigo mingi kwa kutumia barabara hii ya Tabora-Koga-Mpanda.” ameongeza Mrindoko