iNaibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew ameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi mkoani Katavi, ambapo katika kazi ya kukusanya taarifa mkoa huo umefikia asilimia 97.62.
Akizungumza mkoani Katavi wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji na uhamasishaji wa operesheni ya anwani za Makazi, Naibu Waziri Kundo amesema mkoa huo unastahili kupongezwa kutokana na utekelezaji wa operesheni hiyo ikiwa ni pamoja na matumizi mazuri ya fedha.
“Hadi Aprili 25, 2022 mkoa wa Katavi umetekeleza kazi hii ya kukusanya taarifa kwa wastani wa asilimia 97.62 ambapo halmashauri zote zimetekeleza kazi hii kwa zaidi ya asilimia 90 zikiongozwa na halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe, Mlele na Tanganyika zilizotekeleza kwa zaidi ya asilimia 100, nawapongeza sana kwa mafanikio haya.” amesema Naibu Waziri Kundo na kuongeza kuwa
“Nimeridhika na utekelezaji wa anwani za makazi katika mkoa huu, pia mmefanya vizuri kwa kuonesha mchanganuo wa mapato na matumizi ya fedha katika utekelezaji wa zoezi hili, pia ni vizuri kuhakikisha Wakaguzi wa Ndani kupitia halmashauri zetu wanaangalia matumizi ya fedha.”
Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Katavi, Mwamvua Mrindoko amesema kuwa licha ya mafanikio hayo kumekuwepo na changamoto kadhaa ikiwemo mwitikio mdogo wa wananchi juu ya utengenezaji wa vibao na nguzo kwa ajili ya makazi na bararabara au mitaa.