Kardinali Rugambwa apokelewa kwao Kagera

0
330

Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa ameungana na wananchi wa mkoa Kagera katika hafla ya kumpongeza na kumkaribisha nyumbani Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, baada ya kuteuliwa na kusimikwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Kardinali.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Kijiji cha Kasheshe, Nyaishozi wilayani Karagwe, Waziri Bashungwa amewasilisha salamu za Rais akisema “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaungana na Watanzania kuendelea kumpongeza Kardinali kwa heshima hii ambayo nchi yetu tumeipata, amenipa dhamana ya wizara ya ujenzi na baada ya kuona mawasiliano barabara ya kuja hapa Kasheshe yalivyokuwa, sisi tulijiongeza ili tusimuangushe Rais tukatengeneza barabara ili wageni watakaotoka sehemu mbalimbali wafike hapa kwa urahisi kwa kumpongeza Kadinali,” alisema Bashungwa.

Kwa Upande wake, RC Mwassa alisema Mkoa wa Kagera una bahati sana kwani umeweza kumtoa Kardinali na hiyo ni heshima ya kipekee ambayo itasaidia mkoa wa Kagera kuwa na wacha Mungu na kuepuka yote yaliyokatazwa kwenye maandiko matakatifu.

Naye, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa aliwashukuru wananchi wa Kagera kwa kumpokea na kuwasihi Watanzania kuendelea kumtegemea Mungu kwa kila jambo ili waweze kuvuna mema.