Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amezikaribisha kampuni za Ufaransa kuja kuwekeza nchini Tanzania hususan katika sekta za kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Sita ikiwemo ujenzi wa miundombinu, kilimo, elimu, afya na utalii.
Hayo yameainishwa wakati wa mazungumzo kati ya Dkt. Mpango na Shirikisho la Wafanyabiashara wa Ufaransa (MEDEF) Paris, Ufaransa.
Makamu wa Rais amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inachukua hatua mbalimbali kuboresha mazingira ya uwekezaji na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uchumi wa Tanzania na hivyo uwekezaji wao utakuwa katika mikono salama.
Aidha, Makamu wa Rais aliwafahamisha wafanyabiashara hao baadhi ya jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ili kuvutia wawekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kisasa kama Reli ya Mwendokasi (Standard Gauge Railway), mradi wa umeme wa Julius Nyerere utakaozalisha megawati 2115, miradi ya maji na uboreshaji wa miundombinu ya barabara na usafiri wa anga.
Kampuni hizo zilionesha kuridhishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuahidi ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa miradi ya kipaumbele.
Aidha, kama ishara ya kuunga mkono jitihada hizo, Kampuni hizi zilifahamisha kuwa zinatarajia kufanya ziara nchini Tanzania kabla ya mwisho wa mwaka 2021 ili kuangalia fursa za uwekezaji.
Baadhi ya Kampuni kubwa za Ufaransa zilizoshiriki mazungumzo hayo ni pamoja na TOTAL ÉNERGIES na AIRBUS ambazo tayari zimefanya uwekezaji mkubwa nchini.