Kampuni ya Wilmar International ya nchini Singapore imesema ipo tayari kupanua uwekezaji wake katika uzalishaji wa mchele na mafuta hapa nchini, kwa kuwa mchele wa Tanzania ni bora na una soko kubwa duniani na mahitaji ya mafuta ni makubwa ndani ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kampuni hiyo Kuok Khoon Hong wakati wa mazungumzo yake na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es salaam.
Amesema kampuni ya Wilmar International imefurahishwa na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwavutia zaidi wawekezaji, na kwamba tayari imewekeza dola milioni 150 za Kimarekani katika kiwanda cha kusafisha mafuta ya kupikia, kutengeneza sabuni pamoja na tambi ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa takribani dola bilioni moja za Kimarekani Barani Afrika.
Kwa sasa kampuni ya Wilmar imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kukoboa mpunga na kufungasha mchele mkoani Morogoro, kitakachokuwa na uwezo wa kukoboa tani 300 za mpunga kwa siku na kutoa ajira kwa watu zaidi ya 300.
Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza kampuni ya Wilmar International kwa uwekezaji wake hapa nchini, na ameikaribisha kupanua zaidi uwekezaji huo hasa katika uzalishaji na usindikaji wa mafuta ya alizeti, michikichi na kilimo cha umwagiliaji.
Amemueleza Mwenyekiti wa kampuni hiyo Kuok Khoon Hong kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na kampuni hiyo katika uwekezaji huo na ameagiza wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango kuandaa andiko la pamoja na kampuni hiyo litakalowezesha ushirikiano huo hususan katika kupata teknolojia, mbegu na mitaji.