Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia yazinduiwa

0
209

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro
amesema lengo la kampeni ya Kitaifa ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni kuimarisha upatikanaji wa haki kwa umma.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Dkt. Ndumbaro amesema, kampeni hiyo pia inalenga kuimarisha
utoaji wa msaada wa kisheria kwa kutumia jitihada za kuongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususani haki za wanawake na kuimarisha huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.

Ameongeza kuwa jitihada zaidi zinahitajika ili kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu elimu ya sheria kwa umma, elimu katika masuala ya haki na wajibu na kuifahamu misingi ya utawala bora.

Kwa mujibu wa Dkt. Ndumbaro, dhamira ya serikali ni kujenga jamii yenye usawa mbele ya sheria, jamii ambayo inaheshimu na kuthamini utu wa kila mmoja kuanzia mtoto hadi mzee.

Kampeni ya Kitaifa ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia itatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa ushirikiano wa wizara zenye dhamana, taasisi za kiserikali, mashirika yanayotoa msaada wa kisheria pamoja na wadau wa maendeleo ya jamii kwa ujumla.