Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Maafa na Kinyonga, Kilwa Kivinje mkoani Lindi, wameishukuru serikali kwa kuwafikishia chanjo ya UVIKO – 19 katika maeneo yao.
Chanjo ya UVIKO 19 imefikishwa katika vijiji hivyo
kupitia kampeni Harakishi inayotekelezwa na taasisi ya Mkapa Foundation.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walipokuwa wakipatiwa chanjo hiyo, wakazi hao wamesema kampeni hiyo inayofanyika nyumba kwa nyumba imewarahisishia wananchi wanaoshindwa kufika vituo vya kutolea huduma kupata chanjo kwa urahisi.
Afisa mradi anayesimamia kampeni hiyo
kutoka taasisi ya Mkapa Foundation Dkt. Nangaghe Mgweno amesema, tayari wametekeleza kampeni hiyo kwa mafanikio katika wilaya za Ruangwa na Kilwa.
Amesema wamekuwa wakifika katika maeneo hatarishi na yale ambayo ni magumu kufikika ili kuhakikisha wakazi wa maeneo hayo wanapata chanjo ya UVIKO 19.
Kampeni Harakishi inatekelezwa kwa muda wa siku 9 wilayani Kilwa na inasimamiwa na Taasisi ya Mkapa Foundation kwa kushirikiana na wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).