Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imesema uchunguzi wake umebaini kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe hakusema uongo bungeni kama ambavyo ilidaiwa na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina.
Hayo yameelezwa bungeni leo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kondoa Mjini, Ally Makoa wakati akiwasilisha maoni ya kamati juu ya ushahidi wa Mpina kuthibitisha tuhuma zake dhidi ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuwa alilipotosha Bunge kwa kusema uongo.
Juni 4 mwaka huu wakati Waziri Bashe akitoa ufafanuzi kuhusu suala la upungufu wa sukari nchini, Mpina alisimama bungeni na kusema kwamba maelezo aliyoyatoa waziri kuhusu kiasi cha upungufu wa sukari, na maelezo kwamba hadi Januari mwaka huu hakuna kampuni iliyopewa kibali cha kuingiza sukari kwamba ni uongo.
Mpina alieleza kuwa waziri alidanganya kwa kusema upungufu wa sukari kwa mwaka 2022/2023 ulikuwa tani 60,000. Alitoa ushahidi kuwa Bodi ya Sukari ilieleza kuwa upungufu wa sukari ni tani 30,000. Waziri katika utetezi wake alileta ushahidi wa muhtasari wa kikao ambacho kiliidhinisha upungufu wa sukari wa tani 30,000 na akiba ya tani 30,000 hivyo kufanya jumla ya upungufu wa tani 60,000 za sukari.
Kamati baada ya kupitia vielelezo hivyo ilijiridhisha kuwa maelezo na vielelezo vya Mpina yalikuwa sahihi kwa upande wa upungufu wa sukar na maelezo ya waziri hayakulipotosha bunge kwa kuwa aliongelea upungufu wa sukari pamoja na akiba ya sukari.
Aidha, Mpina alimtuhumu waziri kwa kutoa vibali vya tani 410,000 kinyume na upungufu wa sukari ulioidhinishwa wa tani 100,000. Kamati imesema waziri alieleza kuwa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Sukari ilibaini upungufu ni tani 220,000 hadi Aprili, 2024. Hata hivyo, kutokana na tathmini iliyofanywa na wizara ilibainika kuwa uzalishaji uliathirika kutokana na mvua za El-Nino na kutokana na uhaba uliokithiri kwa miezi ya Januari na Februari, 2024 nchi ilihitaji kuwa na uhakika wa sukari kwa ziada (buffer stock), hivyo kuidhinisha makisio ya upungufu wa sukari wa tani 410,000.
Kamati imeridhika kuwa kiwango cha tani 100,000 alichokisema Mpina ni makisio yaliyofanyika mwezi Desemba mwaka 2023. Kiwango hicho kilifanyiwa marejeo Aprili, 2024 na kupelekea ongezeko la upungufu wa sukari kutoka tani 155,000 hadi tani 220,000.
Kiwango cha tani 410,000 alizozisema waziri zilijumuisha mahitaji yaliyokadiriwa mwezi Aprili na tathmini iliyofanyika baadaye iliyobaini kuwa hadi Mei, 2024 viwanda havikuwa vimeanza uzalishaji hivyo mahitaji pamoja na ziada kufikia Desemba, 2024 ni tani 410,000 na hivyo kutoa idhini ya tani hizo.
Aidha, kamati imebaini kwamba ni kweli kwamba kampuni ambazo waziri alizitaja kuwa zilipewa vibali vya kuingiza sukari hazikuwa zimeingiza sukari lakini madai ya Mpina kuwa kwa kusema hivyo waziri alidanganya si sahihi.
Kwa muktadha huo, kamati imesema kuwa maelezo ya waziri aliyoyatoa bungeni yalikuwa sahihi na hakudanganya Bunge au kusema uongo kama ambavyo Mbunge Luhaga Mpina alivyodai.