Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameridhia kuongeza muda wa siku saba kwa kamati maalum iliyopewa jukumu la kuchunguza mauaji yaliyofanyika Mtwara na Kilindi, Tanga.
Kamati hiyo iliyoanza kazi Februari 4, 2022 ilipaswa kukamilisha ripoti yake ndani ya siku 14, zilizoishia Februari 17, 2022. Lakini kutokana na ukubwa wa kazi na mahitaji ya kujiridhisha na baadhi ya masuala, kamati imeomba kuongezewa siku saba kuanzia Februari 17 hadi Februari 23, 2022.
Kamati hiyo iliundwa na Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Februari 4, 2022 wilaya Magu, Mwanza akiwa njiani kuelekea Mkoani Mara kwenye maadhimisho ya miaka 45 ya CCM.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa mamlaka husika kuendelea kutoa ushirikiano kwa kamati ili iweze kuikamilisha kazi hiyo kwa wakati na ufanisi