Kamati : Usimamizi wa chakula urejeshwe TMDA

0
246

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeishauri serikali kufanya tathmini ya kina ya usimamizi wa masuala ya chakula ili kurejeshwa chini ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) na hivyo kurahisisha utendaji kazi na kusimamia usalama wa chakula nchini.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Aloyce Kamamba mara baada ya kamati kufanya ziara katika ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa, Mwanza.

“Ni vyema wizara ya Afya pamoja na wizara ya Viwanda na Biashara izikutanishe kamati hizi mbili na kutoa ushauri ambao unakidhi mahitaji ya sasa huduma hizi kuwa sehemu moja.” amesema Kamamba

Ameongeza kuwa masuala ya dawa na chakula ni maeneo yanayofanana ukichukua kwa upande wa chakula usimamizi uko Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na dawa ziko TMDA.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Sera na Mipango ya wizara ya Afya
Tumainieli Macha amesema, hadi mwaka 2018 masuala ya usimamizi wa chakula yalikuwa chini ya TFDA (TMDA kwa sasa) kabla ya kuhamishiwa kwenda TBS.

Amesema serikali imeanza kufanya mapitio upya ya usimamizi wa masuala ya chakula ili kuboresha upatikanaji wa huduma na kuongeza usimamizi wa masuala ya chakula na dawa nchini.