Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imesema kuwa mradi wa Mabasi yaendayo haraka mkoani Dar es Salaam unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo udhaifu katika mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa DART kama vile kukosekana kwa sheria inayosimamia usafiri wa umma mijini na kukosekana kwa mfumo thabiti wa ukusanyaji wa mapato.
Kamati imesema hayo ikiwasilisha taarifa za mwaka za shughuli zake na kuongeza kwamba hali hiyo isiporekebishwa inaweza kukwamisha juhudi za Serikali katika kujenga na kuendeleza uchumi wa kati na maendeleo ya viwanda.
Kwa mujibu wa kamati, mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es salaam unalenga kuwasafirisha watu wengi kwa wakati mmoja ili waweze kufika haraka wanapokwenda nia ikiwa ni kuwawezesha watumiaji wa usafiri huo wafike mapema kwenye shughuli zao za uzalishaji mali na utoaji wa huduma.
Licha ya changamoto, kamati imesema utekelezaji wa mradi huo umechangia kuboresha huduma ya usafiri jijini Dar es salaam.