Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Athuman Ngenya amesema, shirika hilo limepata taarifa ambayo bado inafanyiwa kazi kuhusu poda hususani za watoto zinazomilikiwa na kampuni ya Johnson & Johnson kuhusishwa na kusababisha Saratani.
Akizungumza kwa njia ya simu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
Dkt. Ngenya
amefafanua kuwa poda zilizotajwa kuhusika na Saratani ni zile za toleo maalumu na sio poda zote kama inavyodhaniwa.
Ameongeza kuwa poda za Johnson zilizopo sokoni kwa sasa hapa nchini zinatokea Afrika ya Kusini na tayari TBS
imewasiliana na mamlaka za nchini huko kufahamu kama poda hizo za Johnson zilizopo nchini Tanzania ni toleo hilo linalohusishwa na kusababisha Saratani.
Dkt. Ngenya amewashauri watu wote wanaotumia poda za Johnson & Johnson wasitishe matumizi ya poda hizo na kuziweka pembeni hadi hapo taarifa kamili itakapotolewa na Shirika la Viwango Tanzania.