Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imemwita Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt Imni Patterson kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa masuala yanayoandikwa katika mitandao yake ya kijamii bila ya uthibitisho.
Dkt Patterson amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Wilbert Ibuge jijini Dar Es Salaam.
Katika mazungumzo hayo Balozi Ibuge ameeleza masikitiko yake kutokana na namna ambavyo Ubalozi wa Marekani hapa nchini umekuwa ukitoa taarifa za ushauri wa kiusafiri ikiwemo suala la namna Tanzania inavyoshughulikia ugonjwa wa corona.
Miongoni mwa taarifa zilizotolewa katika mtandao wa Twitter wa ubalozi huo zinaleta taharuki ya Corona kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi ilhali hali halisi siyo kama inavyodaiwa.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amemjulisha Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini kuhusu umuhimu wa Ubalozi kutoa taarifa zilizothibitishwa na serikali.