Mkufunzi kutoka Chuo cha Ualimu Ilonga kilichopo Wilaya ya Kilosa, Morogoro, Liliani Mfikwa amewataka walimu kuwa wachechemuaji mahiri wa utoaji wa huduma ya chakula shuleni kwa kuwa lishe bora ina mchango mkubwa katika kujenga afya ya mwanafunzi, kupunguza utoro, kuongeza usikivu, kuboresha mahudhurio na kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Akibainisha umuhimu wa chakula na lishe shuleni alipokuwa akitoa mafunzo kwenye semina ya walimu wa shule za sekondari wanaohusika na utekelezaji wa programu ya shule salama nchini, Lilian amebainisha kuwa suala hilo limezingatia Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014.
Amesema utoaji wa huduma ya chakula shuleni unapaswa kuhakikisha wanafunzi wote wanapata mlo kamili unaozingatia makundi matano ya vyakula ili kuweza kukabiliana na njaa ya muda mfupi na njaa iliyofichika kwa maana ya mwanafunzi kupungukiwa na baadhi ya virutubisho kama vile madini au vitamin fulani mwililini.