Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Katibu Tawala mkoa huo kuhakikisha dawa zote zilizoko katika baadhi ya hospitali, vituo vya afya na zahanati ambazo zimeisha muda wake wa watumizi na hazijateketekezwa katika halmashauri za mkoa huo ziwe zimeteketezwa.
Kagaigai ametoa muda huo wilayani Hai katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na kuongeza kuwa haiwezekani dawa ziishe muda halafu haziteketezwi mpaka sasa.
Amesema uko umuhimu pia kwa Katibu Tawala kufuatilia sababu ya dawa hizo kuisha muda wake wakati mahitaji ya dawa katika hospitali na vituo vya afya ni makubwa.
Akitoa taarifa ya CAG, Mhasibu wa wilaya ya Hai, Juma Kassoga amesema dawa zenye thamani ya shilingi milioni 43.8 kutoka katika baadhi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali zimeshindwa kuteketezwa katika kipindi cha mwaka 2019/2020.
Hoja ya uwepo wa dawa zilizoisha muda wake na ambazo hazijateketezwa huku zikiwa na thamani ya mamilioni ya fedha imekuwa ikijitokeza katika halmashauri nyingi mkoani Kilimanjaro.