JWTZ yaitwa kuwekeza mkoani Mara

0
216

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee ameliomba Jeshi la Wananchi Tanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizomo mkoani humo ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.

Meja Jenerali ametoa ombi hilo wakati wa mapokezi ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda ambapo amesema mkoa huo una fursa nyingi za uwekezaji lakini bado hazijatumika ipasavyo.

Ametolea mfano kilimo cha umwagiliaji ambapo amesema ipo fursa kubwa kutokana na uwepo wa Ziwa Victoria, lakini inashangaza kuona wakulima mkoani humo wakitegemea mvua kama mikoa isiyo na ziwa.

Ameliomba Jeshi hilo kupitia miradi yake, kuanzisha programu za kilimo cha umwagiliaji ambapo mbali na kukuza uchumi wa jeshi pia itasaidia kuinua uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Jenerali Mkunda ameupongeza mkoa kwa ushirikiano wake na vyombo vya dola huku akiahidi kutumia fursa zilizotajwa kwa maendeleo ya Taifa.

Mkuu wa Majeshi amewasili mkoani Mara kwa ziara ya kawaida na amepata fursa ya kuonana na uongozi wa mkoa kwa majadiliano mafupi.