Rais Samia Suluhu Hassan leo ameshiriki kwa njia ya mtandao kwenye mkutano wa Wakuu wa nchi na mashirika ya Kimataifa uliojadili namna ya kuokoa uchumi wa nchi za Afrika kufuatia madhara yaliyosababishwa na ugonjwa wa corona.
Mkutano huo uliofanyika jijini Paris, -Ufaransa uliandaliwa na Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo na kuhudhuriwa na Marais wa nchi za Angola, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Ivory Coast, Misri, Ethiopia, Ghana, Mali, Mauritania, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Senegal, Sudan, Togo, Tunisia, Italia, Hispania na Umoja wa Ulaya.
Marais wa Tanzania, Kenya, Afrika Kusini, Uholanzi, Ujerumani, China na Japan wameshiriki kwenye mkutano huo wa njia ya mtandao.
Mashirika ya Kimataifa yaliyoshiriki ni Umoja wa Mataifa, Shirika la Fedha la Kimataifa, Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo Duniani, Shirika la Biashara Duniani na Benki ya Dunia.
Wakati wa mkutano huo, Rais Samia Suluhu Hassan ameungana na Marais wengine duniani kumpongeza Rais Macron kwa kuitisha mkutano huo, ambao wamesema umelenga sio tu kusaidia uchumi wa Bara la Afrika bali kuokoa maisha ya binadamu waliopo Afrika kutokana na kuathirika na madhara yaliyosababishwa na corona.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania kama zilivyo nchi zingine duniani imekumbwa na madhara ya ugonjwa wa corona, ambayo yameathiri biashara, utoaji wa huduma za kijamii, kushuka kwa mapato, kupoteza maisha na kupoteza ajira mambo ambayo yamewaathiri zaidi Wanawake, Vijana na Watoto.
Amebainisha kuwa kutokana na athari hizo, Tanzania ambayo hivi karibuni imeingia katika uchumi wa kipato cha kati imechukua hatua mbalimbali ili kulinda uchumi wake na hasa miradi mikubwa ya kimkakati inayoitekeleza ikiwemo kuimarisha zaidi mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji zaidi nchini.
Ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo hususani Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua stahiki kuokoa uchumi wa nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na mashirika ya fedha ya kimataifa kuongeza mikopo yenye masharti nafuu kwa miradi ya maendeleo ya nchi za Afrika na kusaidia sekta binafsi katika Bara hilo kwa kuiwezesha kupata mikopo nafuu ili kukuza biashara hasa ndogo na za kati ambazo ndio nguzo muhimu ya uchumi.
Rais Samia Suluhu Hassan ametaja hatua nyingine kuwa ni kusamehe mikopo ama kuongeza muda wa ulipaji wa mikopo ambayo nchi za Afrika zinadaiwa, na kuchangia fedha katika bajeti za nchi za Afrika kutokana na nchi hizo kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.