JPM atoa siku 7 kukamilika Daraja la Kiyegeya

0
363

Rais John Magufuli ametoa siku saba kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, na Mawasiliano kukamilisha ujenzi wa Daraja la Kiyegeya linalounganisha mikoa ya Morogoro na Dodoma.

Ametoa agizo hilo leo wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa daraja hilo mkoani Morogoro ambapo pia amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo kuwasiamisha kazi wahusika wote 12 waliofanya ukaguzi wa barabara kuhakikisha zinapitika.

“Ndani ya siku saba nataka magari yawe yanapita kwa speed (kasi) hapa,” ameagiza Rais.

“Nchi hiyo wahandisi waliosajiliwa wako 25,000 hawana kazi, halafu watu wanapewa kazi wanakuja kufanya upumbavu. Waziri unda katume kadogo (sio kakutumia pesa) uchunguze economic effects (athari za kiuchumi) iliyosababishwa na hawa watu,” ameagiza Rais Magufuli.

Aidha, amemuonya waziri mwenye dhamana na kusema kwamba onyo alilotoa leo ni la mwisho kwani alitaka kumfukuza kazi kutokana na uzembe uliofanywa na wataalamu hao ambao umepelekea nchi kupata athari za kiuchumi.

Daraja hilo lilikatika Machi 2 mwaka huu na kusababisha adha za usafiri kwa maelefu ya watu wanaotumia barabara hiyo.