JPM aagiza kufanyika uchunguzi kuhusu vipimo vya corona

0
489

Rais John Magufuli amemuagiza Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Dkt Mwigulu Nchemba kufanya uchunguzi kuhusu umakini katika Maabara ya Taifa iliyopewa jukumu la kupima virusi vya corona kutokana na kuwepo kwa utata katika majibu ya sampuli mbalimbali.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati wa hafla fupi ya kumuapisha Dkt Nchemba wilayani Chato mkoani Geita na kuongeza kuwa uchunguzi uliofanywa umebaini sampuli mbalimbali zisizo za binadamu zilizopelekwa katika maabara hiyo kutoa majibu yanayoonesha zina maambukizi ya corona, jambo ambalo linawewezekana si la kweli.

Amemuagiza Waziri Nchemba kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kuhakiki umakini wa vifaa vilivyopo katika maabara hiyo pamoja na uwezo wawataalamu waliopo kwa ajili ya kufanya kazi ya upimaji.

Amesema sampuli mbalimbali zilipelekwa katika maabara hiyo ikiwa ni pamoja na zile za kutoka kwa mbuzi, kondoo, papai na fenesi na majibu yameonyesha baadhi ya vitu hivyo vina maambukizi ya corona.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, awali alikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini na kuwaagiza kuchunguza utendaji kazi wa vipimo hivyo na kukubalia kuchukua sampuli hizo ambazo baadhi majibu yameonesha kuwa na utata.