JKT kuja na mkakati wa kutengeneza ajira kwa wahitimu

0
300
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa akijibu maswali katika kikao cha pili cha mkutano wa tisa wa Bunge la 12.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Innocent Bashungwa amesema Jeshi la Kujenga Taifa litapanua wigo wa kazi kwa kushirikiana na wizara za kisekta kuweka mkakati wa pamoja kutengeneza ajira kwa vijana wanaomaliza mafunzo ya kujitolea katika Jeshi hilo.

Ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Malinyi, Antipas Mgugusi aliyetaka kujua ni lipi agizo la Serikali katika kutoa kipaumbele cha ajira kwa wahitimu wa mafunzo ya JKT.

“Jeshi la Kujenga Taifa tunataka tupanue mawanda kwa kushirikisha sekta nyingine kama Wizara ya Kilimo, Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na taasisi nyingine kuweka mkakati wa kusaidia kutengeneza ajira kwa vijana wanaomaliza mafunzo ya kujitolea na kurudi mtaani.” amesema Bashungwa

Amesema ameunda kamati maalum katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambayo itashirikiana na wizara nyingine za kisekta na taasisi zake na kuja na mkakati wa pamoja wa kuongeza wigo wa ajira za vijana wanaojitolea.

Bashungwa ameeleza kuwa lengo la mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwapatia vijana wa Tanzania elimu ya uzalendo, ujasiriamali na kujifunza stadi za kazi ili waweze kijiajiri mara wanapomaliza mkataba.