JKCI yapata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake

0
217

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo mkoani Dar es salaam imesaidia kupunguza gharama kubwa kwa Wagonjwa wa moyo nchini kwenda kutafuta matibabu nje ya nchi.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo mkoani Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa mtambo mpya wa uchunguzi na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo katika Taasisi hiyo na kuongeza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa JKCI katika kuokoa maisha ya Watanzania.

“Nimeingia humu ndani nimeona mambo makubwa yanafanyika, na sasa hivi Tanzania tunajisifu kwa kupunguza vifo kutokana na matumizi ya mashine ya ugunduzi wa matundu kwenye moyo kabla mtoto hajazaliwa na bila ugunduzi huu wangepotea wengi zaidi.”amesema Rais Samia Suluhu Hassan

Zaidi ya wagonjwa elfu tano wenye hitilafu kwenye moyo wamefanyiwa upasuaji kwenye Taasisi hiyo ya Moyo Jakaya Kikwete huku 11 kati yao ambao ni asilimia 0.2 wamefariki dunia baada ya upasuaji huo.

“Zamani ukisikia umeme kwenye moyo huelewi ni kitu gani lakini sasa uchawi wake umegundulika kupitia teknolojia ya vifaa tiba vya moyo inayotusaidia kuokoa maisha ya watoto wetu wengi.” amesema Rais Samia Suluhu Hassan

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuimarisha huduma za afya nchini kwa ajili ya Watanzania wote.